NAYASHITAKI MAKAMPUNI MANNE YA SIMU

NAYASHITAKI MAKAMPUNI MANNE YA SIMU

Started
24 November 2019
Petition to
MAKAMPUNI YA SIMU TZ. (TANZANIA)
Signatures: 5,714Next Goal: 7,500
Support now

Why this petition matters

Started by Bashir Yakub

BASHIR  YAKUB, Wakili.

0714047241.

Naishitaki Tigo, Airtel, Vodacom na Halotel. Kwa mujibu ya Sheria Namba 12/2003 ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania mashtaka ya aina hii natakiwa kuyaandikia makampuni hayo taarifa kuyataka yarekebishe ndani ya siku 30 ninacholalamikia yakishindwa naendelea mbele, ambapo nimeshayaandikia makampuni hayo. 

Kwenye mashitaka yangu ninaomba mambo matano.

JAMBO LA KWANZA: Vifurushi vyote havipaswi kuexpire. Kitu pekee ambacho kinapaswa kumaliza kifurushi inatakiwa iwe ni wewe kuongea hadi dakika zako zikaisha.

Si haki kukata kifurushi cha mtu ambaye dakika zake za kuongea,za data, au sms bado zipo kwa kigezo cha kuexpire au muda wake wa wiki, masaa12, nk kuisha. Nchi nyingi hii kitu imeondolewa imebaki kwetu na pengine pachache.

Mathalan, umejiunga kifurushi cha 1000 na umepewa dakika 10 ndani ya masaa 12. Umetumia dakika 3 tu ambazo thamani yake kifedha ni shilingi 300, na masaa 12 yameisha. Maana yake kwenye 1000 yako zilibaki dakika 7 ambazo thamani yake kifedha ni shilingi 700, ambazo hizo sasa shilingi 700 kampuni ya simu inajirudishia kwa kigezo cha muda kuexpire. Nachelea kuiita huu wizi lakini initoshe kusema hii haiwezi kuwa haki.

Lakini pia ninapolipa 500 na wewe ukaniuzia kifurushi si nimekulipa hela yako yote na wewe hunidai. Sasa kwanini tena unachukua kilekile nilichonunua kwako na hela yako yote nimeshakulipa. 

Ni hivi,unaponunua kifurushi ni sawa na umenunua bidhaa, na ukishanunua bidhaa hakuna mtu mwingine yeyote, akiwemo aliyekuuzia bidhaa hiyo, mwenye haki ya kuichukua tena bidhaa hiyo yote au sehemu yake isipokuwa wewe uitumie mpaka iishe.

Tizama Tanesco na LUKU. Tanesco akishakuuzia umeme/units ukamlipa basi hatma ya units zako ni utumie mpaka umalize.Hawezi kuikata na kujirudishia kwasababu anajua alikuuzia bidhaa na wewe ukamlipa na hivyo una haki ya kutumia bidhaa yako mpaka umalize. Hii ndiyo HAKI.

Kinachofanywa na makampuni ya simu ni sawa ununue mkate dukani na mwenye duka umlipe hela yake yote. Halafu mwenye duka huyohuyo akwambie kwamba usipokula mkate huo kufikia saa 12 za jioni au ndani wiki au mwezi nitakuja tena kuuchukua nyumbani kwako, na aje kweli auchukue iwe mali yake tena kwa mara ya pili.

Zaidi ya hayo,ukweli halisi ni kuwa kifurushi kwa muundo wake si bidhaa inayoexpire. Ukinunua mkate ukiexpire utauona, utaona kabisa kwa macho umeoza kadhalika bidhaa nyingine zenye sifa ya kuexpire. Lakini kifurushi kwa uhalisi wake si bidhaa inayoexpire au yenye sifa ya kuexpire.

Hili neno kuexpire limetengezwa ili kuficha neno kupora au uporaji. Ukweli ni kwamba kifurushi kinaporwa makusudi kwa kigezo hovyo kabisa na dhahania cha kuexpire, sijui masaa yako 12, sijui wiki yako, sijui mwezi wako umeisha nk. Kifurushi kinaishaje kabla dakika zangu nilizolipia kwa ukamilifu sijazitumia zikaisha ?

Yapo haya nayo lazima yaeleweke, mtu amejiunga lakini yuko safarini hawezi kutumia mda wake, mwingine alipo hakuna network, mwingine hajatumia mda wake alikuwa bize na kazi zake, mwingine simu haikuwa na chaji siku nzima, mwingine umeme ulikatika alikosa mawasiliano nk nk, hawa wote pesa zao walizolipia na hawajazitumia au wametumia kidogo zinakatwa na makampuni ya simu yanajirudishia pesa hizo bila kujali.

Nimefungua kesi kuondoa unyonyaji huu na lazima uondoke.Hatuwezi kuendelea kuwa viwanda vya kutengeneza ukwasi wa makampuni ya simu.

JAMBO LA PILI: Haki ya kutochanganyiwa kifurushi na muda wa kawaida wa maongezi bila ridhaa.

Nitatoa mfano, unakuta mtu ameweka shilingi 1000 kwenye simu ambapo anajiunga 500 na 500 inabaki kama muda wa maongezi wa kawaida. Wakati anapokuwa akizungumza au akitumia data kupitia ule muda aliojiunga na ukaisha basi simu haikatiki bali inaunganisha moja kwa moja na ile 500 ya muda wa maongezi wa kawaida ambayo alikuwa hajajiunga.

Hii si sawa hata kidogo na ni vitu ambavyo vinatengenezwa maksudi ili kujipatia fedha bila kujali mtumiaji anaumia kiasi gani. Ni hivi, mtu anapoamua kujiunga 500 na akabakisha 500 bila kuiunga ana maana yake kubwa tu.Hakushindwa kuunganisha 1000 yote.Amechagua 500 kwa maksudi maalum. Sasa iweje unamlazimisha kutumia akiba yake ya 500 hata bila ridhaa yake.

Inatakiwa kuwe na chaguo (option) iwapo mtu anahitaji huduma ya aina hiyo au hapana. Au inatakiwa muda wa kifurushi ukiisha simu ikate halafu kama anataka kuendelea kutumia muda wa kawaida achague mwenyewe kuendelea kuutumia na sio kampuni ya simu kumchagulia.

Au kama anataka kujiunga na hiyo 500 iliyobaki basi ajiunge. Isiwe biashara ya kuviziana kama ilivyo sasa. Hili nalo lazima waliondoe.

JAMBO LA TATU: Haki ya kujua matumizi ya kifurushi.Malalamiko ya vifurushi vya watu kuliwa isivyo kawaida ni mengi mno.

Unanunua dakika 20 unaongea 10 unaambiwa kifurushi kimeisha, unabaki kushangaa. Ni lazima waweke mfumo wenye kutoa taarifa sahihi na za wazi (transparency) ili kumwezesha mtumiaji kumonita matumizi ya kifurushi chake.

Malalamiko ya watu ya kutumia vifurushi chini ya kile walichonunua yanaongezeka siku hadi siku. Kuwaachia makampuni ya simu wao wawe ndio wauzaji wa vifurushi, na wao hao hao ndio wakueleze umetumia nini,kama umemaliza au hujamaliza, huku wewe mteja ukiwa kipofu/gizani ukisubiri kupokea lolote wanalolisema wao, kupigwa hakuwezi kukwepeka.

Waweke mfumo ambao wao pamoja na mteja watamonita matumizi ili mteja aweze kuhoji. Teknolojia imekua hili ni dogo sana.

JAMBO LA NNE: Haki ya kuhamisha kifurushi.

Nimesema hapo juu kifurushi ni mali yako na ndo maana unailipia pesa na hivyo kuwa na haki ya kuitumia kwa uhuru.

Kwa msingi huu makampuni ya simu ni lazima yaweke mfumo unaomwezesha mtu kumhamishia mtu mwingine kifurushi kama ilivyo kwenye muda wa kawaida wa maongezi. Maana yake nikinunua kifurushi cha 1000 labda dakika 10 za maongezi, Mb 100, na sms 50.

Niwe na uwezo wa kumgawia yeyote ninayemtaka kiasi cha muda wangu wa maongezi,sms au Mb. Na hii inafanyika nchi nyingi na inawezekana zaidi kugawiana watu wa mtandao mmoja.Tunahitaji uhuru huu kwetu.

JAMBO LA TANO: Haki ya kupewa tahadhari kuhusu kifurushi au muda wa hewani unapokaribia kuisha. Kuna makampuni wana huduma hii lakini wanaitoa kwa hiari sana na wengine wameacha kabisa. Wengine wanatoa tahadhari muda unapoisha na sio unapokaribia.

Tunataka watoe unapokaribia ili mtu ajipange. Ni haki mtu kupewa tahadhari wakati akizungumza,akiwa kwenye mtandao, au sms, kuhusu dakika zake kukaribia kuisha. Sio sahihi wala ustaarabu simu kukatika ghafla bila tahadhari.

 Na wanafanya hivyo maksudi wakijua unapokatakiwa na mawasiliano ghafla ni lazima tu utakuwa hujamaliza haja yako na hivyo utalazimika kuongeza vocha ili umalizie na wao wapate mauzo zaidi.

Wanajua ukipewa tahadhari unaweza tu kufupisha mazungumzo yako na wakati simu inakatika ukawa tayari umemaliza na hivyo usihitaji tena kuongeza vocha. Tabia za hovyo kabisa za kuviziana.

Unawezaje kunipa tahadhari ya muda kuisha ukashindwa kunipa ya muda kukaribia kuisha. Hili nalo tunataka lifanyiwe kazi.

SHERIA

Mambo haya kwa ujumla wake ni kinyume na Katiba ya JMT Ibara ya 18 (c) inayotaka uwepo wa mawasiliano bila kuingiliwa, lakini yanakiuka Kanuni za Kielektroniki na Mawasilano ya Posta kuhusu viwango vya Tozo GN. No 22/2018 hasa Kanuni ya 4 (1 na 2) inayotaka viwango vyote vya tozo za simu kuwa vya haki na kadri(just and reasonable), yanakiuka Kanuni ya 4 ya Kanuni za Kielektroniki na Mawasiliano ya Posta GN No.61/2018 kuhusu kumlinda mlaji inayotaka mlaji kupewa taarifa kwa usahihi ya matumizi ya huduma muda wote, yanakiuka Sheria ya Ushindani namba 8/2003 inayotaka mtoa huduma kutoa huduma kwa kuzingatia zaidi maslahi ya watu wa hali ya chini, na sheria nyingine nyingi zimekiukwa.

Na tuelewane vizuri hapa, hakuna kitu kinaitwa VIGEZO NA MASHARTI KUZINGATIWA. Sheria iko wazi kuwa neno, maneno, sentensi au msemo wowote wenye lengo la kusigina haki ya mtu/watu ni batili.

Basi nitaviomba vyombo vya maamuzi vitusaidie kuyaweka sawa haya matano.Tutazidi kupeana taarifa kadri inavyokwenda.

Support now
Signatures: 5,714Next Goal: 7,500
Support now
Share this petition in person or use the QR code for your own material.Download QR Code

Decision-Makers

  • MAKAMPUNI YA SIMU TZ.TANZANIA